Thursday, September 15, 2016

Faida za Boda-boda



Faida za Boda-Boda.

Nilianza kuendesha pikipiki kunako mwaka 1992, ilikuwa Honda C70 iliyotengenezwa mwaka 1980. Kabla ya kutumia pikipiki safari za mjini zilikuwa ni tatizo haswa kwa vile ni kilometa 3 hadi mjini katikati na kuna kilima kilichojificha barabara ya Lema, hivyo safari ya kurudi nyumbani huwa ni ngumu. Wakati jua likiwa kali inabidi kufikiria mara mbili mbili kabla ya kupanga safari yoyote. Katika barabara hii kulikuwa hakuna usafiri wa mabasi, isipokuwa yale yaendayo Kibosho Kirima, kama matatu au manne kwa siku. Niliendelea kutumia hiyo piki piki hadi Septemba 2005 ilipoibiwa.


Kipindi hicho, baada ya kuibiwa nikawa ninatafuta ingine ya kununua. Kukawa na piki piki za CC 125 kwa sh 600,000 za kutoka China. Hizi piki piki za bei rahisi zilikuwa dalili ya nafasi ambayo imekuwa ikijijenga; yaani ajira kwa vijana wa Watanzania. Kuanza kwa biashara ya usafiri wa piki piki imewapa wananchi fursa ya kuwa na usafiri wa bei nafuu ambao pia unaweza kupita sehemu ambazo barabara siyo nzuri. Bei ya chombo cha usafiri ni ndogo, haswa ukilinganisha na bei ya piki piki ya CC 125 ya Honda ambayo miaka ya 1990 ilikuwa inalingana na Toyota Pick ya tani moja second hand kutoka Japan.

Kwa sasa, kuna takriban piki piki 1,000,000 hapa Tanzania, ikilinganishwa na takriban magari 880,000. Nchi ya China imekuwa ikiendeleza vyombo ya usafiri / uchukuzi  vidogo kwa muda mrefu. Vyombo hivi ni vya teknologia rahisi na pia vinaweza kutengenezwa kwa bei ndogo na kuuzwa kwa bei ndogo. Vyombo ya magurudumu 3 vimekuwa vikitumika huko China kwa muda mrefu. Swala hili la vyombo vya usafiri vya bei ndogo limepitiwa na nchi za ulaya pia, haswa baada ya vita vya pili vya dunia. Mifano ni piki piki za Vespa huko Italia. India waliona faida za piki piki za magurudumu matatu, na ni nchi inayoongoza kwa usafiri wa vyombo hivyo.

Sisi Watanzania tulianza kugeukia teknologia rahisi kunako mwaka 1980, wakati trekta dogo (Power Tiller) lilipotengengenezwa hapa nchini. Baada ya hapo wazo halikuendelezwa. Hadi kufikia awamu ya nne, ambapo ilikuwa sera ya serikali kuendeleza matumizi ya Power Tiller kwaajili ya kilimo. Hivyo muongo wa kwanza (2000 – 2010) umekuwa ndiyo mwamko wa tektnologia rahisi kwa matumizi ya umma nchini Tanzania, Boda-boda na Power Tiller. Ukijumlisha simu za mkononi na Solar Power, hizi ndiyo zinazoainisha maedeleo yetu ya sasa.

Maendeleo tutajiletea sisi wenyewe, tukitumia teknologia zilizopo na haswa zile ambazo zinaendana na mazingira yetu (Appropriate technology), tutaweza kujijengea maisha mazuri na yenye mfanikio.  

Faida za Usafiri wa Piki piki ni hizi:
1. Piki piki ni za bei ya chini.
2. Zinatoa ajira kwa vijana wa Tanzania.
3. Bei ya usafiri ni ya chini.
4. Piki piki zinaweza kufika maeneo yenye barabara mbovu.
5. Sekta ya Boda-boda inachangia uchumi.

Mapungufu ya Usafiri wa Piki piki ni hizi:
1. Madereva wa Boda-boda hawana mafunzo ya udereva.
2. Idadi kubwa ya piki piki hazilipiwi Motor Vehicle Licence.
3. Idadi kubwa ya piki piki hazilipiwi Third Party Insurance.
4. Baadhi ya madereva wa Boda-boda hawana maadili, utu na uadilifu.
5. Vijana wengi wamepoteza viungo na maisha.

William Makupa
14 September 2016