Faida za Boda-Boda.
Nilianza kuendesha pikipiki kunako mwaka
1992, ilikuwa Honda C70 iliyotengenezwa mwaka 1980. Kabla ya kutumia pikipiki
safari za mjini zilikuwa ni tatizo haswa kwa vile ni kilometa 3 hadi mjini
katikati na kuna kilima kilichojificha barabara ya Lema, hivyo safari ya kurudi
nyumbani huwa ni ngumu. Wakati jua likiwa kali inabidi kufikiria mara mbili
mbili kabla ya kupanga safari yoyote. Katika barabara hii kulikuwa hakuna
usafiri wa mabasi, isipokuwa yale yaendayo Kibosho Kirima, kama matatu au manne
kwa siku. Niliendelea kutumia hiyo piki piki hadi Septemba 2005 ilipoibiwa.
Kipindi hicho, baada ya kuibiwa nikawa
ninatafuta ingine ya kununua. Kukawa na piki piki za CC 125 kwa sh 600,000 za
kutoka China. Hizi piki piki za bei rahisi zilikuwa dalili ya nafasi ambayo
imekuwa ikijijenga; yaani ajira kwa vijana wa Watanzania. Kuanza kwa biashara
ya usafiri wa piki piki imewapa wananchi fursa ya kuwa na usafiri wa bei nafuu
ambao pia unaweza kupita sehemu ambazo barabara siyo nzuri. Bei ya chombo cha
usafiri ni ndogo, haswa ukilinganisha na bei ya piki piki ya CC 125 ya Honda
ambayo miaka ya 1990 ilikuwa inalingana na Toyota Pick ya tani moja second hand
kutoka Japan.
Kwa sasa, kuna takriban piki piki
1,000,000 hapa Tanzania, ikilinganishwa na takriban magari 880,000. Nchi ya
China imekuwa ikiendeleza vyombo ya usafiri / uchukuzi vidogo kwa muda mrefu. Vyombo hivi ni vya
teknologia rahisi na pia vinaweza kutengenezwa kwa bei ndogo na kuuzwa kwa bei
ndogo. Vyombo ya magurudumu 3 vimekuwa vikitumika huko China kwa muda mrefu.
Swala hili la vyombo vya usafiri vya bei ndogo limepitiwa na nchi za ulaya pia,
haswa baada ya vita vya pili vya dunia. Mifano ni piki piki za Vespa huko
Italia. India waliona faida za piki piki za magurudumu matatu, na ni nchi
inayoongoza kwa usafiri wa vyombo hivyo.
Sisi Watanzania tulianza kugeukia
teknologia rahisi kunako mwaka 1980, wakati trekta dogo (Power Tiller)
lilipotengengenezwa hapa nchini. Baada ya hapo wazo
halikuendelezwa. Hadi kufikia awamu ya nne, ambapo ilikuwa sera ya serikali
kuendeleza matumizi ya Power Tiller kwaajili ya kilimo. Hivyo muongo wa kwanza
(2000 – 2010) umekuwa ndiyo mwamko wa tektnologia rahisi kwa matumizi ya umma
nchini Tanzania, Boda-boda na Power Tiller. Ukijumlisha simu za mkononi na
Solar Power, hizi ndiyo zinazoainisha maedeleo yetu ya sasa.
Maendeleo tutajiletea sisi wenyewe, tukitumia
teknologia zilizopo na haswa zile ambazo zinaendana na mazingira yetu (Appropriate technology), tutaweza
kujijengea maisha mazuri na yenye mfanikio.
Faida za Usafiri wa Piki piki ni hizi:
1. Piki piki ni za bei ya chini.
2. Zinatoa ajira kwa vijana wa Tanzania.
3. Bei ya usafiri ni ya chini.
4. Piki piki zinaweza kufika maeneo
yenye barabara mbovu.
5. Sekta ya Boda-boda inachangia uchumi.
Mapungufu ya Usafiri wa Piki piki ni
hizi:
1. Madereva wa Boda-boda hawana mafunzo
ya udereva.
2. Idadi kubwa ya piki piki hazilipiwi
Motor Vehicle Licence.
3. Idadi kubwa ya piki piki hazilipiwi Third
Party Insurance.
4. Baadhi ya madereva wa Boda-boda
hawana maadili, utu na uadilifu.
5. Vijana wengi wamepoteza viungo na
maisha.
William Makupa
14 September 2016