Friday, June 30, 2017

Hitler, Chama cha Nazi na Dola ya Tatu ya Ujerumani


ADOLF HITLER, CHAMA CHA NAZI NA DOLA YA TATU YA UJERUMANI

Mwanzo
Adolf Hitler alizaliwa katika kijiji cha Braunau am Inn huko Austria kunako 20 Aprili 1889. Baba yake alikuwa ni Alois Hitler ambaye alifanya kazi ya Afisa Ushuru wa Forodha kwenye mpaka wa Austria na Ujerumani. Hitler alipokea komunyo ya kwanza kunako mwaka 1904 na akaacha shule 1905.

Hitler akiwa mtoto mdogo

 
Hitler akiwa mtoto

Hitler aliacha shule na akawa ni mzururiaji katika mji wa Linz. Alijaribu kujiunga na masomo ya sanaa ya uchoraji lakini hakufaulu mitihani ya kujiunga (1907). Akawa anachora Postcard kwaajili ya kuuza na kwa kuwa hakuwa na kipato kizuri, mara nyingi alilazimika kulala na kula kwenye makazi ya kijamii ya wasio na makazi, hali hii ilidumu miaka 5. Hali yake ya maisha haikuwa nzuri hadi pale ilipoanza Vita vya Kwanza vya Dunia, kunako 28 Julai 1914. Ni vizuri ikaeleweka kuwa katika bara la Ulaya, kuanza kwa Vita vya Kwanza vya Dunia kulipokelewa kwa furaha na watu wengi. Sababu za kufurahia kuanza kwa vita zilikuwa ni nafasi ya nchi kuonyesha umahiri wake, wanaume kuweze kujiendeleza kijamii, wanaume kuweza kujiendeleza kiuchumi, nafasi ya kujaribisha silaha mpya na vile vile kurekebisha mipaka ya nchi. Hadi kufikia 1914, vita vya nchi za ulaya havikuwa na na majeruhi wengi hivyo maafa makubwa yalikuwa bado hajaonekana, kwa mfano silaha ya Maxim Machinegun ilikuwa hajawahi kutumika kwa kiasi kikubwa katika vita barani Ulaya hadi 1914.  

Hitler akishangilia kutangazwa kwa Vita vya Kwanza vya Dunia huko Odeonplatz Vienna


 
Hitler wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, ni wa kwanza kulia.

Nchi ya Austria
Vita hivi vilimpa Hitler nafasi ya kuonyesha ujasiri wake, alijiunga na jeshi la Ujerumani na siyo la nchi yake Austria. Nchi ya Austria ilikuwa ni sehemu ya Dola ya Austria Hungary tangu mwaka 1867. Nchi hii iliongozwa na Mfalme Francis Joseph wa ukoo wa Habsburg-Lorraine, watawala wa jadi wa Dola Takatifu ya Rumi. Dola ya Austria Hungary ilikuwa ni mkusanyiko wa mataifa mengi chini ya milki ya Mfalme Francis Joseph, mataifa haya ni pamoja na Austria, Hungary, Bosnia, Czech, Slovakia, Slovenia na Romania.

Nchi ya Ujerumani
Kama Dola ya Austria ilikuwa muunganiko wa nchi mbalimbali kwa njia ya vita, kurithi au ndoa, nchi ya Ujerumani ilichukua picha iliyonayo sasa kunako 1871 baada ya kushinda vita dhidi ya Ufaransa. Ushindi huu uliiruhusu Dola ya Prussia chini ya Mfalme Wilhem von Hohenzollern kuunganisha majimbo huru ya Kijerumani kuwa Shirikisho Moja. Ieleweke kuwa Majimbo Huru ya Kijerumani yalikuwa na histroria tofauti na pia mifumo tofauti ya utawala, kilichawaunganisha ni lugha moja ya Kijerumani. Austria au Osterreich (Dola ya Mashariki) ilikuwa ina nguvu sana na haikweza kumezwa na Prussia kunako 1871.  

Kuoteshwa kwa Mbegu ya Vita vya Pili vya Dunia
Ilipofika tarehe 11 Novemba 1918, Vita vya Kwanza vya Dunia vilisimama rasmi, baada ya Ujerumani kukubali kushindwa. Jambo hili la kukubali kuwa wameshindwa vita na hasa masharti magumu ya kulipishwa gharama za vita na kulazimishwa kukubali kuwa ndiyo waanzilishi ya vita katika Mkutano wa Amani wa Versailles, vilipelekea kuoteshwa kwa mbegu ya Vita vya Pili vya Dunia. Sehemu ya jeshi la Ujerumani na wananchi pia waliona kuwa baadhi ya viongozi na wanasiasa walisaliti na kulazimishia Ujerumani kujitoa katika vita na kuomba kusimamishwa kwa mapigano. Dhana hii ilijulikana kama Usaliti wa Kuchoma Kisu Mgongoni. Ikimaanisha wakati askari wa kijerumani wanapigana vita na adui, wengine waliwasaliti kwa kuwachoma mgongoni pale ambapo walitegemea msaaada na siyo usaliti.  

 
Hitler baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia

Vita, kulipia gharama za vita kwa nchi zingine na vurugu za kisiasa za wakomunisti kujaribu kuhodhi madaraka kulipelekea kuwepo na hali ya vurugu na mporomoko wa kiuchumi nchini Ujerumani. Katika hali hii, askari jeshi wa mrengo wa kulia waliunda jeshi la mgambo la kulinda amani na kuzuia wakomunisti kuhodhi madaraka. Wakomunisti walipindua serikali ya jimbo la Bavaria na kuliendesha kwa muda. Mfumo wa demokrasia wa uwakilishi wa kiwango na mporomoko wa kiuchumi kuliifanya Jamhuri wa Weimar (Jamhuri ya Weimar iliundwa baada ya Mfalme Wilhelm kujiuzulu na Ufalme kufutwa) kuwa dhaifu na kuwa na uwezo mdogo wa kutawala. Haya yote hayakumfurahisha Adolf Hitler, na katika kipindi hiki 1919 alijiunga na Chama Cha Wajamaa wa Kitaifa, kikijulikana kwa kifupi kama Chama cha Nazi. Alikuwa mtu wa saba kujiunga na chama hicho.

 
Hitler mwanzo wa kazi za kisiasa

Baada ya muda mfupi alitwaa madaraka ya chama cha Nazi na akawa kiongozi wa hicho chama. Alitumia muda mwingi kati ya 1921 na 1923 kupiga propaganda za kisiasa za mrengo wa kulia za kukanusha kuwa Ujerumani ilishindwa Vita vya Kwanza vya Dunia, kulaani kulipishwa gharama za vita, kupiga vita ukomunisti na ni kipindi hiki ambapo alianza sera za chuki dhidi ya Wayahudi. Kwa utamaduni wa Bavaria, unywaji wa bia ni jadi na Hitler alikuwa anahubiri sera zake kwenye kumbi za kunywea bia.  

Mahangaiko Yangu
Ilipofikia mwaka 1923 Novemba 8 na 9, Hitler pamoja na Herman Goring wakihusisha maafisa wengine wa mrengo wa kulia walijaribu kupindua serikali ya jimbo la Bavaria. Mapinduzi haya ya kijeshi hayakufanikiwa na Hitler akajikuta anatumikia kifungo cha miaka mitano katika gereza la Landsberg. Kwa kuwa porojo za mahubiri zilizidi gerezani, mmoja wa wafungwa alimshauri labda angeandika Kumbukumbu Zake badala ya kuwapigia kelele, kwa vile gerezani mtu hawezi kuondoka kupisha kelele za mwingine. Hiki ndicho kikawa chanzo cha kuandikwa kwa kitabu cha Mein Kampf, yaani Mahangaiko Yangu. Katika kitabu hiki Hitler aliainisha mipango yake, sera na itikadi za mrengo wa kulia, kuchukia demokrasia na kuwachukia Wayahudi. Aliachiwa mapema baada ya miezi tisa tu, 20 Desemba 1924.

Kuteuliwa kuwa Chancellor
Harakati za kisiasa ziliendelea baada ya kuachiwa huru mapema. Kunako mwaka 1929 uchumi wa dunia nzima uliporomoka baada ya bei za hisa kuporomoka katika Soko la Hisa la New York. Sakata hili lilifanya hali ya kisiasa nchini Ujerumani kuwa ngumu zaidi, ni katika mazingira haya, na haswa baada ya Hitler kuomba msamhaha kwa Rais Hindenburg, Franz von Papen aliwezesha Hitler kuteuliwa kuwa Reich Chancellor wa Ujerumani (30 Januari 1933). Katika mfumo wa utawala wa Ujerumani, Chancellor ni mkuu wa serikali lakini siyo mkuu wa dola. Kikundi kilichompendekeza Hilter ateuliwe kuwa Chancellor kilifikiri kuwa kingeweza kumwendesha kwa urahisi, awe kibaraka wao. Jambo ambalo hawakulitegemea ni kutumika kwa Jeshi la SA kuzuia wabunge kuingia bungeni na kupiga kura, mkakati huu ulipelekea kuzuiwa kwa upinzani bungeni na kurahisisha utawala wa Hitler.   

 
Hitler na Himmler wanakagua Jeshi la SS

Mizizi ya Udikteta
Baada ya muda mfupi Hitler alidai apewe kifaa cha kisheria cha kumwezesha kutekeleza sera zake, na Sheria ya Kumwezesha (23 na 24 Machi 1933) itapitishwa ambapo hakuhitajika kuleta kila jambo kujadiliwa mbele ya bunge. Hatua hii ni ukiukwaji wa taratibu za utawala na zilipelekea kukua kwa udikteta. Inaaminika kuwa Goring aliwasha moto jengo la bunge, Reichstag tarahe 27 Februari 1933 ili kuleta msukosuko wa kisiasa na Sheria ya Moto wa Reichstag iliyokabidhi serikali mamlaka ya bunge. Marinus van der Lubbe raia wa Holland alisingiziwa kuwa amewasha moto huo kwa hulka zake za kikomunisti, swala hili lilitumika kuwazuia wabunge wakomunisti kuingia bungeni na wengi waliwekwa kizuizini.

Kuwa Fuhrer
Mwaka 1934, Hitler aligombania uraisi dhidi ya Field Marshal Paul von Hindenburg. Hitler alishindwa katika uchaguzi huu, lakini Hindenburg alipofariki yeye Hitler aliunganisha cheo cha Chancellor and Rais akawa Kiongozi (Fuhrer). Chama cha Nazi kilikuwa na wanagambo wake wajulikanao kama Wenye Mashati ya Brown (Jeshi la Dhoruba), au SA, jeshi hili lilikuwa chin ya uongozi wa Ernst Rohm. Shida ilijitokeza kuwa yeye Rohm alionekana kama tatizo kwa Hitler na mbinu zikafanyika akasingiziwa kuwa alitaka kupindia serikali. Rohm na wenzake waliuwawa kwenye kile kinachojulikana kana Usiku wa Visu Virefu. Baada ya hapa, Jeshi la SS (Jeshi la Ulinzi) likawa ndiyo linaongoza katika nyanja zote za usalama na ulinzi wa Hitler. Pia ilimpa nafasi Heinrich Himmler kupanda cheo na kuwa wanne kutoka kwa Hitler. Wapili alikuwa Rudolf Hess na watatu Goring.

 
Horthy na Hitler huko Kiel 1938

Kuanzia mwaka 1935, Hitler alitoa makucha yake na kupitisha Sheria za Kibaguzi za Nuremberg. Na mwaka 1936 alipeleka majeshi katika eneo la Rhineland. Jambo hili lilikuwa limezuiliwa na Mkataba ya Amani wa Versailles wa 1919. Jumuiya ya Madola haikichukua hatua zozote na Hitler akachukulia kama kibali cha kuanza kujenga jeshi la Ujerumani (Wehrmacht) na kuanza utengenezaji was silaha.

Kumezwa kwa Austria
Ujasiri wa Hitler uliendela kuongezeka, na mwaka 1938 alilazimisha kuungana kwa Ujerumani na Austria (Anschluss).  Baada ya muda, wajerumani wa Sudetenland huko Czechoslovakia walianza kudai kuwa wananyanyaswa. Malalamiko yao yalikuwa yamepangwa na viongozi wa ki-Nazi kutoka Ujerumani, kwa kibali cha Mkutano wa Munich ulioitishwa na Mussolini na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Neil Chamberlain, Hilter aliteka eneo la Sudetenland la Czechoslovakia. Kunako tarehe 9 Novemba 1938, Dr Joseph Goebbels alitumia Jeshi la SA kuharibu maduka ya raia wenye asili ya Kiyahudi na kuchoma masinagogi nchini Ujerumani kama jibu la mwanafunzi mwenye asili ya kiyahudi kumuua mwanadiplomasia wa Kijerumani mjini Paris. Uvunjwaji huu wa maduka na biashara unajulikana kama Usiku wa Vioo vya Kuchonga. Jambo ambalo halikufikiriwa vizuri na waliopanga udhalimu huu ni kuwa biashara nyingi zilikuwa zimekatiwa bima, hivyo uchumi wa nchi ulilipia huu uharibifu wa kupangwa.

Kuanza kwa Vita vya Pili vya Dunia
Huu utaratibu wa kumridhisha Hitler ulimfanya aendelee kuongeza madai ya ardhi barani Ulaya, na mwaka 1939 alidai Ujerumani ikabidhiwe eneo la Silesia lililoko Poland na kuwa na kipande cha ardhi cha kuunganisha Prussia ya Mashariki na Ujerumani kupitia bandari ya Danzig (Danzig Corridor). Madai haya hayakukubaliwa na Uingereza na Ufaransa, badala yake nchi hizi mbili zikaweka Mkataba wa Kudhamini Uhuru wa Poland. Hivyo Ujerumani ilipovamia Poland kunako saa 11 asubuhi tarehe 1 Septemba 1939, nchi ya Uingereza na Ufaransa viliitaka Ujerumani iondoe majeshi yake Poland na hadi kufikia tarehe 3 Septemba 1939 na baada ya Ujerumani kushindwa kutii masharti ya “Ultimatum” ya nchi zote mbili, dunia ikajikuta katika vita tena.

 
Hitler na Goring

Kushindwa kwa Ufaransa
Wakati nchi ya Poland inaendelea kumezwa na Ujerumani na kufuatia Mkataba wa Molotov Ribbentrop (23 Agosti 1939), Poland Mashariki ilivamiwa na majeshi ya Kirusi na maafisa 22,000 wa Poland waliuwawa kwa amri za Joseph Stalin, dikteta wa Kisovieti katika Msitu wa Katyn. Huku kwenye uwanja wa mapambano wa Ufaransa na Uingereza hakukuwa na mapigano yoyote na dhana ya “Phoney War” ikajijenga. Hivi vita vya ukimya viliendelea hadi mwaka 1940 wakati jeshi la Werhmarcht lilipokuwa tayari kushambulia Ufaransa kupitia Ubeljiji, mbinu ya kivita ambayo ilitumika pia kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia (Schlieffen Plan). Jeshi la Wehrmarcht pia lilitumia mbinu ya Shambulio la Radi (Blitzkrieg). Blitzkrieg ilileta mafanikio dhidi ya Poland na kufikia mwezi June 1940, nchi ya Ufaransa ilikubali kushindwa na kusalim amri ya Hitler. Hitler aliigawa Ufaransa katika sehemu mbili, kaskazini ikawa Ufaransa Iliyotekwa (Occupied France) na kusini ikawa Ufaransa ya Kibaraka (Vichy France) chini ya Marchal Petain. Wakati Ufaransa inasalimu amri ya Hitler, majeshi ya Kiingereza yalitoroka kupitia bandari ya Dunkirk. Hitler aliamuru kuwa Mkataba wa Kukubali Kushindwa Vita wa Ufaransa uwekwe sahihi katika behewa lilelile ambalo lilitumika mwaka 1918 dhidi ya Ujerumani kwenye Msitu wa Compiegne, na baada ya hapo alilipua lile behewa la treni ili lisije kutumika tena.   

 
Reichsmarschall Herman Goring, Mkuu wa Jeshi la Anga (Luftwaffe)

Pambano la Uingereza
Baada ya Ufaransa kushindwa vita, hatua iliyofuata ilikuwa kushambulia Uingereza kwa ndege, pambano linalojulikana kama Pambano la Uingereza (Battle of Britain). Vita hivi vilipiganwa kwa Jeshi la Anga la Ujerumani (Luftwaffe) kutupa mabomu kwenye miji ya Kiingereza na Jeshi la Anga la Uingereza (Royal Air Force) kutungua ndege za kutupa mabomu (Bomber Aircraft) kwa kutumia mizinga ya ardhini (Anti Aircraft Machinegun) au ndege za uwindaji (Fighter Aircraft). Ushindi wa Uingereza katika pambano hili ulitokana na uongozi dhabiti wa Winston Churchill, ndege za Spitfire and ujasiri pamoja na nia ya wana-anga. Jeshi la Luftwaffe lilikuwa linaongozwa na Reichsmarschall Herman Goring

Tabaka Tawala
Ilipofika mwaka 1941, Hitler akaamuru matayarisho ya kuivamia Urusi. Kulikuwa na malengo matatu, la kwanza ni kuiondoa Urusi kama nchi inayoweza kuwa tishio kwa Ujerumani, pili ni kwamba Hitler alikuwa anachukia itikadi ya kikomunisti na tatu alitaka ardhi ya Urusi kwaajili ya kuifanya koloni la Kijerumani (Lebensraum). Hii ni dhana ya kwamba kuna binadamu wa aina mbili, Herrenfolk (Master Race) inayoundwa na Wajerumani na Wascandinavia. Wazungu wenye nywele za njano na macho ya bluu. Aina ya pili ni Untermenschen (Sub-human) ambayo ni nusu binadamu, inayoundwa na watu wengine wote kasoro ya Wafaransa, Waitalia na mataifa mengine ya wazungu ambao siyo Slavic. Falsafa na itikadi hii inammanisha kuwa Hitler alikuwa na mpango wa kuwafanya binadamu wote kuwa watumwa wa Tabaka la Juu. Tarehe 22 Juni 1941 jeshi la Werhmarcht lilivamia nchi ya Urusi na kufanya maafa makubwa. Siku za mwanzoni za vita Werhmarcht ilipata ushindi baada ya ushindi na kunako mwaka 1941 walifika karibu na mji mkuu wa Moscow (Krasnaya Polyana, 28 Novemba 1941, kilomita 29 kutoka Kremlin).

General February
Vita dhidi ya Urusi vilifanya rasilimali za Ujerumani zitumike kwa kiasi kikubwa sana, hasa kwasababu ya ukubwa wa eneo. Joseph Stalin aliamuru viwanda vyote vikubwa vilivyopo magharibi vihamishiwe mashariki, jambo lilichangia uwezo wa Urusi kuendele na vita. Nchi yoyote inayopigana na Urusi ni lazima izingatie jambo moja muhimu, nalo ni kipindi cha kipupwe kinachoanza November hadi March kila mwaka. Hivyo jeshi la Wehrmarcht lililazimika kusimamisha mapigano kwenye kipindi cha kipupwe 1941 / 1942. Jeshi halikuwa tayari kwa mazingira ya baridi kali, kama ambavyo Napoleone Bonaparte hakuwa tayari mwaka 1812, miaka 129 iliyotangulia. Ilipofika kipupwe cha 1942 / 1943 ikawa wazi kuwa Ujerumani haitaweza kuiangamiza Urusi, na tarehe 31 Januari 1943 Field Marshal Fredrich von Paulus alisalimisha wanajeshi 93,000 wa Werhmarcht kwa majeshi ya Urusi. Hitler alimhitaji apigane mpaka askari wa mwisho atakapo kufa. Na alimpandisha cheo kutoka General kuwa Field Marshal ili ajiue kuliko kijisalimisha. Kati ya askari 93,000 (au 87,000) waliochukuliwa mateka Stalingrad Januari 1943 ni 5000 tu ndiyo waliorudi nyumbani baada ya 1945.

 
Reichsfuhrer SS Heinrich Himmler


Mauaji ya Wayahudi
Kwa maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Reichsfuhrer SS Heinrich Himmler, kiliitishwa kikao huko Wansee nje ya Berlin kujadili swala la watu wenye asili ya Kiyahudi. Kama mwanzoni ilifikirika kuwa labda wangeweza kurudishwa Palestina, na baadaye ikafikirika wangepelekwa Madagascar (Baada ya Ufaransa kushindwa vita), katika kikao hiki cha 1942 uhamuzi wa kuwaua wote ulikuwa umeshachukuliwa, na kikao kilikuwa na kazi ya kujadili njia za utekelezaji. Kuwapiga risasi ilionekana ni kuchezea rasilimali ghali wataki wa vita, na pia iliwadhuru askari kisaikologia kuua wanawake na watoto. Gesi ya carbon monoxide haikuwa na ufanisi mkubwa, na pia haikuua watu wote. Hivyo kikao kikashauri kutumika kwa dawa ya kuua wadudu Zyklon B yenye cynanide. Kambi za Mauaji (Death Camps) zikatengenezwa na watu wote ambao walionekana kuwa hawafai walipelekwa huko kwaajili ya kuuwawa.

 
Kambi ya Kusindika Watu

Kulikuwa na kambi za aina mbili, ya kwanza ni Kambi za Kusindika Watu (Concentration Camps) na aina ya pili ni Kambi za Mauaji. Watu walisafirishwa na treni kwenye mabehewa ya mizigo (Box Car) bila ya chakula au maji kutoka kwenye Kambi za Kusindika Watu kwenda kwenye Kambi za Mauaji. Walipofika kwenye Kambi ya Mauaji, walichaguliwa kwenda kufanya kazi za kitumwa (Forced Labour) au kwenda kwenye vyumba vya gesi (Gas Chamber). Wazee, watoto, wagonjwa, vilema na baadhi ya wanawake walipelekwa moja kwa moja kuuwawa. Walivuliwa nguo, wakakatwa nywele na baadaye kufungiwa kwenye chumba cha gesi ambapo makopo yenye Zyklon B yalitumbukizwa kwa juu na kutoa gesi ya sumu. Baada ya kelele za watu kutulia, wafungwa maalum wajulikanao kama Sonderkommando waliitoa ile miili ya marehemu, wakaingoa meno ya dhahabu au fedha, wakaiweka kwenye matanuru ya moto na kuichoma. Majivu yalitupwa kwenye mito au yalitengenezea mbole ya chumvi chumvi. Mali za marehemu zilichambuliwa, na vilivyoweza kutumika vilitumika. Kwa njia hii takriban Wayahudi million sita waliangamizwa pamoja na Gypsies (Kabila la Wazururaji wa Ulaya).  

 
Kambi za Mauaji, uchomaji wa miili ya watu.

Nje ya mauaji katika Kambi za Mauaji, pia kulifanyika mauaji katika misitu huko Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine. Mauaji haya yalifanya na jeshi la SS, ambapo raia wenye asili ya kiyahudi na makada ya kikomunisti walivuliwa nguo wakapigwa risasi na kutupwa kwenye mashimo makubwa (Mass Graves). Na kwa vile jambo hili lilifanyika kwa uwazi, wale waliokuwa wanasubiri waliona kitakacho wasibu kabla ya kuuwawa. Vikosi vya Mauaji Einsatzgruppen vilihama kutoka sehemu moja hadi ingine kutekeleza sera hii ya udhalimu chini ya uongozi wa Reinhard Hydrich. Kinachosikitisha ni kuwa ilipoonekana dalili kuwa Ujerumani itashindwa vita, Himmler alamuru haya makaburi yachimbuliwe na mateka wa vita halafu ile miili ichomwe moto kuharibu ushahidi.

 
Himmler na Jeshi la SS

Kuhodhi Madaraka ya Kijeshi
Mwaka 1943 ulishuhudia Pambano la Kursk, pambano kubwa la vifaru, mahali ambapo ubora wa kifaru cha Kirusi cha T-34 ulidhihirika. Wakati huu baada ya mabishano mengi na makamanda ya jeshi, Hitler alitwaa cheo cha mkuu wa jeshi la nchi kavu (Oberster Befehlshaber des Herres). Alimstaafisha amri jeshi mkuu wa Werhmarcht, Field Marshal Walter von Brauchitsch (19 Desemba 1941). Awali aliunda Ober Kommando der Werhmarcht (OKW) chini ya amri yake ikiongozwa na Field Marshal Wilhelm Keitel and Colonel General Alfred Jodl baada ya kufuta Wizara ya Ulinzi na kumstaafisha waziri wa ulinzi Field Marshal Werner von Blomberg kunako 4 Februari 1938. Ikumbukwe kuwa Hitler hakujipansha cheo, alibaki na cheo chake cha Lance Corporal.   

Kushindwa Vita
Mwaka 1944, kunako tarehe 6 June, majeshi wa washirika yalivamia pwani ya Normandy Ufaransa na kufungua mlango wa mwisho wa utawala wa Hitler, Vita vya Pili vya Dunia na Dola ya Tatu ya Ujerumani (Third Reich). Vikosi vya vifaru vilishindwa kudhibiti shambulio hilo hadi Hitler alipoamka saa nane mchana, jambo lililosaidia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa zoezi hilo la Wamarekani, Waingereza and Wafaransa. Hitler alitegemea shambulio lingekuja Pas de Calle, lakini hakuwa hivyo. Licha ya jitihada kubwa, mji wa Paris ulianguka mikononi mwa Washirika, baada ya hapo uvamizi wa Ujerumani ukaanza. Katika hali hii Wajerumani walikuwa wanapigana na Warusi kwa upande wa mashariki, Waserbia, Wakroatia na Wayunani katika peninsula ya Balkan, Waingereza na Wamarekani katika peninsula ya Italia na Ulaya magharibi. Katika mazingira haya, kikundi cha mmafisa wa Werhmarcht wakahamua kummua Hitler, Colonel Stauffenberg alitega bomu chini ya meza ya Hitler huko Wolfsschanze Rastenburg Prussia ya Mashariki tarehe 20 Julai 1944. Kwa bahati kuna mtu alisogeza bomu upande mwingine was meza na hivyo halikumuua Hitler lilipolipuka. Baada ya hapo maaskari wengi walinyongwa kulipiza kisasi dhidi ya usaliti huo. Dhoruba hii ilimkumba pia Field Marshal Erwin Rommel, kamanda mahiri wa Wehrmarcht huko Afrika ya Kaskazini. Alilazimika kunywa sumu.

Kifo cha Hitler
Kambi ya Mauaji ya Auschwitz ilitekwa na Warusi kunako tarehe 27 Januari 1945, na baada ya hapo Ujerumani ikaendelea kupoteza ardhi katika kila pambano. Alipofariki Rais Roosevelt wa Marekani, Waziri wa Propaganda Joseph Goebbels alisheherekea akifikiri kuwa labda Ushirika dhidi ya Ujerumani ungeyumba, lakini haikuwa hivyo. Kwasababu ya mabomu yaliyokuwa yanadondoshwa kila siku, Hitler alilazimika kuhamia kwenye handaki chini ya Reich Chancellery, mahali ambapo alisheherekea sikukuu ya kuzaliwa tarehe 20 Aprili 1945 na mwishowe akafunga ndoa na Eva Braun na kujiua kwa kunywa sumu na kujipiga risasi kunako tarehe 30 Aprili 1945. Siku za mwisho za Dola ya Tatu zilishuhudia udhalimu dhida ya Wajureumani wenyewe uliofanywa na Jeshi la SS, ambapo kila mwanaume aliyeshukiwa kuwa ametoroka uwanja wa mapambano alinyongwa papo hapo, Waziri wa Viwanda Alber Speer aliagizwa alipue miundombinu yote ili Warusi wasikute chochote cha thamani, Speer hakutekeleza agizo hili. Herman Goring alituma telegram ya kutaka kuchukua madaraka ya uongozi, jambo ambalo Goebbels aliligeuza kuwa ni usaliti, Hitler akaamuru Goring awekwa kuzuizini. Himmler naye alitaka kuwa kujadili kusimamisha mapigano na Washirika ili ayaendeleze dhidi ya Warusi, kupitia kwa Count Folke Bernadotte, jambo hili halikufanikiwa, na Hitler alipogundua akaagiza Himmler akamatwe mara moja.    

 
Eva Braun, mke wa Hitler

Uzushi
Joseph Stalin hakutaka kuamini kuwa Hitler amekufa, hivyo akaendeleza wazo kuwa labda alikimbia. Baada ya Hitler na Eva Braun kujiua, miili yao ilichomwa moto na lita 180 za petroli na kuzikwa kwenye bustani ya Reich Chancellery. Warusi walichimbua hiyo miili na baadaye wakaizika mahali pengine, sehemu ya fuvu la kichwa na taya ya Hitler kilipelekwa Moscow. Kunako mwaka 1970 miili ilichimbuliwa tena na kutupwa kwenye mto Biederitz ili kuondoa uwezekano wa kuwa sehemu ya kumsujudu Hitler. Nyumba ya Hitler, Berghof kule Obersalzberg karibu na Berchtesgaden ilibomolewa na dalili zote kufutwa. Mali zake zote zikakabidhiwa Jimbo la Bavaria. Vita vya Pili vya Dunia viliisha rasmi tarehe 7 na 8 Mei 1945. Ni tarehe mbili kwa vile sahihi ya tarehe 7 haikutambuliwa na Warusi itakabidi zoezi lirudiwe siku inayofuata tarehe 8 Mei 1945.      

Matokeo ya Vita vya Pili vya Dunia
1. Kuundwa kwa Umoja wa Mataifa baada ya Jumiya ya Madola kushindwa kuzuia vita.
2. Kuwepo kwa ncha mbili katika dunia, Magharibi ya Ubepari na Demokrasia na Mashariki ya Ujamaa na Udikteta.
3. Kuundwa kwa bomu la Atomiki na kutumika huko Hiroshima na Nagasaki.
4. Kuzuiwa kwa Ujerumani na Japan kusababisha vita tena.
5. Kuzinduliwa kwa Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa 1948.
6. Mauaji ya Wayahudi milioni sita.
7. Takriban watu milioni 50 walikufa kutokana na vita hivi.
8. Kuanzishwa kwa Dola ya Israel 1949.
9. Kusisitizwa kwa itikadi ya watu kujuhamulia mambo yao wenyewe (Self Determination) na kupelekea uhuru wa makoloni.
10. Uhuru wa nchi nyingi ulipelekea maendeleo ya kielimu, kiafya, kijamii na kiteknologia.
11. Vita vilionekana kama udhalimu na hakujakuwa na vita kubwa tena tangu tarehe 7 / 8 Mei 1945.
12 Kwa kila siku ya siku 1400 ambazo Urusi ilukuwa katika hali ya vita na Ujerumani, ilipoteza watu 19,000.


23 April 2017

Wahusia Wakuu
1. Adolf Hitler: Reich Chacellor wa Ujerumani (Sawasawa na Waziri Mkuu) na baadaye Kiongozi Mkuu wa Ujerumani (Fuhrer).
2. Herman Goring: Waziri wa Jeshi la Anga (Luftwaffe) na Reichsmarschall.
3. Heinrich Himmler: Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Gestapo (Askari Kanzu) na Reichsfurhrer wa Jeshi la Ulinzi la SS.
4. Joseph Goebbels: Waziri wa Propaganda.
5. Joseph Stalin: Katibu Mkuu wa Cahama cha Kikomunisti cha Urusi na Kiongozi Mkuu wa Urusi ambaye hakuwa na cheo cha kiserikali.
6. Winston Churchill: Waziri Mkuu wa Uingereza aliyeendesha mapigani dhidi ya Hitler.
7. Benito Mussolini: Warizi Mkuu wa Italia.
8. Vyacheslav Molotov: Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi.
9. Joachim von Ribbentrop: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani.
10. Eva Braun: Mke wa Hitler.


Vyanzo
1. Alan Bullock. Adolf Hitler. Iasi. Editura Elit. 2000.
2. J.P Stern. Hitler: The Fuhrer and the People. Fontana Collins. October 1976.
3. James Joll. Europe since 1870: An International Histroy. Penguin. 1976.
4. Nyiszli Miklos. Am Fost Medic la Auschwitz: Morti Fara Morminte, Laboratorul si Crematoriile Dr-uli Mengele. Editura Aquila 93. 1998.
5. Dragos Nedelescu. Goebbels Jurnal. Iasi. Editura Elit. 1998.
6. Marian Podkowinski. Hitler and Archangles of Death. Cluj Napoca. Hiparion. 2001.
7. Hugh Trevor-Roper. The Last Days of Hitler. 7th Edition. London. Pan Books. 2012.