Historia ya Ukoo wa Makupa wa Mamba Kokirie
Ujuzi na Ujuaji
Monday, November 15, 2021
Friday, June 30, 2017
Hitler, Chama cha Nazi na Dola ya Tatu ya Ujerumani
ADOLF HITLER, CHAMA CHA NAZI NA DOLA YA TATU YA
UJERUMANI
Mwanzo
Adolf Hitler alizaliwa katika kijiji cha
Braunau am Inn huko Austria kunako 20 Aprili 1889. Baba yake alikuwa ni Alois
Hitler ambaye alifanya kazi ya Afisa Ushuru wa Forodha kwenye mpaka wa Austria
na Ujerumani. Hitler alipokea komunyo ya kwanza kunako mwaka 1904 na akaacha
shule 1905.
Hitler akiwa mtoto mdogo
Hitler akiwa mtoto
Hitler aliacha shule na akawa ni
mzururiaji katika mji wa Linz. Alijaribu kujiunga na masomo ya sanaa ya
uchoraji lakini hakufaulu mitihani ya kujiunga (1907). Akawa anachora Postcard
kwaajili ya kuuza na kwa kuwa hakuwa na kipato kizuri, mara nyingi alilazimika
kulala na kula kwenye makazi ya kijamii ya wasio na makazi, hali hii ilidumu
miaka 5. Hali yake ya maisha haikuwa nzuri hadi pale ilipoanza Vita vya Kwanza
vya Dunia, kunako 28 Julai 1914. Ni vizuri ikaeleweka kuwa katika bara la
Ulaya, kuanza kwa Vita vya Kwanza vya Dunia kulipokelewa kwa furaha na watu
wengi. Sababu za kufurahia kuanza kwa vita zilikuwa ni nafasi ya nchi kuonyesha
umahiri wake, wanaume kuweze kujiendeleza kijamii, wanaume kuweza kujiendeleza
kiuchumi, nafasi ya kujaribisha silaha mpya na vile vile kurekebisha mipaka ya
nchi. Hadi kufikia 1914, vita vya nchi za ulaya havikuwa na na majeruhi wengi
hivyo maafa makubwa yalikuwa bado hajaonekana, kwa mfano silaha ya Maxim
Machinegun ilikuwa hajawahi kutumika kwa kiasi kikubwa katika vita barani Ulaya
hadi 1914.
Hitler wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, ni wa kwanza kulia.
Nchi ya Austria
Vita hivi vilimpa Hitler nafasi ya
kuonyesha ujasiri wake, alijiunga na jeshi la Ujerumani na siyo la nchi yake Austria.
Nchi ya Austria ilikuwa ni sehemu ya Dola ya Austria Hungary tangu mwaka 1867.
Nchi hii iliongozwa na Mfalme Francis
Joseph wa ukoo wa Habsburg-Lorraine,
watawala wa jadi wa Dola Takatifu ya Rumi. Dola ya Austria Hungary ilikuwa ni
mkusanyiko wa mataifa mengi chini ya milki ya Mfalme Francis Joseph, mataifa
haya ni pamoja na Austria, Hungary, Bosnia, Czech, Slovakia, Slovenia na
Romania.
Nchi ya Ujerumani
Kama Dola ya Austria ilikuwa muunganiko
wa nchi mbalimbali kwa njia ya vita, kurithi au ndoa, nchi ya Ujerumani
ilichukua picha iliyonayo sasa kunako 1871 baada ya kushinda vita dhidi ya
Ufaransa. Ushindi huu uliiruhusu Dola ya Prussia chini ya Mfalme Wilhem von Hohenzollern kuunganisha majimbo huru ya
Kijerumani kuwa Shirikisho Moja. Ieleweke kuwa Majimbo Huru ya Kijerumani
yalikuwa na histroria tofauti na pia mifumo tofauti ya utawala,
kilichawaunganisha ni lugha moja ya Kijerumani. Austria au Osterreich (Dola ya
Mashariki) ilikuwa ina nguvu sana na haikweza kumezwa na Prussia kunako 1871.
Kuoteshwa kwa Mbegu ya Vita vya Pili vya
Dunia
Ilipofika tarehe 11 Novemba 1918, Vita
vya Kwanza vya Dunia vilisimama rasmi, baada ya Ujerumani kukubali kushindwa.
Jambo hili la kukubali kuwa wameshindwa vita na hasa masharti magumu ya
kulipishwa gharama za vita na kulazimishwa kukubali kuwa ndiyo waanzilishi ya
vita katika Mkutano wa Amani wa
Versailles, vilipelekea kuoteshwa kwa mbegu ya Vita vya Pili vya Dunia.
Sehemu ya jeshi la Ujerumani na wananchi pia waliona kuwa baadhi ya viongozi na
wanasiasa walisaliti na kulazimishia Ujerumani kujitoa katika vita na kuomba
kusimamishwa kwa mapigano. Dhana hii ilijulikana kama Usaliti wa Kuchoma Kisu Mgongoni. Ikimaanisha wakati askari wa
kijerumani wanapigana vita na adui, wengine waliwasaliti kwa kuwachoma mgongoni
pale ambapo walitegemea msaaada na siyo usaliti.
Hitler baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia
Vita, kulipia gharama za vita kwa nchi
zingine na vurugu za kisiasa za wakomunisti kujaribu kuhodhi madaraka
kulipelekea kuwepo na hali ya vurugu na mporomoko wa kiuchumi nchini Ujerumani.
Katika hali hii, askari jeshi wa mrengo wa kulia waliunda jeshi la mgambo la
kulinda amani na kuzuia wakomunisti kuhodhi madaraka. Wakomunisti walipindua
serikali ya jimbo la Bavaria na kuliendesha kwa muda. Mfumo wa demokrasia wa
uwakilishi wa kiwango na mporomoko wa kiuchumi kuliifanya Jamhuri wa Weimar (Jamhuri ya Weimar iliundwa baada ya Mfalme
Wilhelm kujiuzulu na Ufalme kufutwa) kuwa dhaifu na kuwa na uwezo mdogo wa
kutawala. Haya yote hayakumfurahisha Adolf Hitler, na katika kipindi hiki 1919
alijiunga na Chama Cha Wajamaa wa Kitaifa, kikijulikana kwa kifupi kama Chama
cha Nazi. Alikuwa mtu wa saba
kujiunga na chama hicho.
Hitler mwanzo wa kazi za kisiasa
Baada ya muda mfupi alitwaa madaraka ya
chama cha Nazi na akawa kiongozi wa hicho chama. Alitumia muda mwingi kati ya
1921 na 1923 kupiga propaganda za kisiasa za mrengo wa kulia za kukanusha kuwa
Ujerumani ilishindwa Vita vya Kwanza vya Dunia, kulaani kulipishwa gharama za
vita, kupiga vita ukomunisti na ni kipindi hiki ambapo alianza sera za chuki
dhidi ya Wayahudi. Kwa utamaduni wa Bavaria, unywaji wa bia ni jadi na Hitler
alikuwa anahubiri sera zake kwenye kumbi za kunywea bia.
Mahangaiko Yangu
Ilipofikia mwaka 1923 Novemba 8 na 9,
Hitler pamoja na Herman Goring
wakihusisha maafisa wengine wa mrengo wa kulia walijaribu kupindua serikali ya jimbo
la Bavaria. Mapinduzi haya ya kijeshi hayakufanikiwa na Hitler akajikuta
anatumikia kifungo cha miaka mitano katika gereza la Landsberg. Kwa kuwa porojo
za mahubiri zilizidi gerezani, mmoja wa wafungwa alimshauri labda angeandika
Kumbukumbu Zake badala ya kuwapigia kelele, kwa vile gerezani mtu hawezi
kuondoka kupisha kelele za mwingine. Hiki ndicho kikawa chanzo cha kuandikwa
kwa kitabu cha Mein Kampf, yaani
Mahangaiko Yangu. Katika kitabu hiki Hitler aliainisha mipango yake, sera na
itikadi za mrengo wa kulia, kuchukia demokrasia na kuwachukia Wayahudi.
Aliachiwa mapema baada ya miezi tisa tu, 20 Desemba 1924.
Kuteuliwa kuwa Chancellor
Harakati za kisiasa ziliendelea baada ya
kuachiwa huru mapema. Kunako mwaka 1929 uchumi wa dunia nzima uliporomoka baada
ya bei za hisa kuporomoka katika Soko la
Hisa la New York. Sakata hili lilifanya hali ya kisiasa nchini Ujerumani
kuwa ngumu zaidi, ni katika mazingira haya, na haswa baada ya Hitler kuomba
msamhaha kwa Rais Hindenburg, Franz
von Papen aliwezesha Hitler kuteuliwa kuwa Reich
Chancellor wa Ujerumani (30 Januari 1933). Katika mfumo wa utawala wa
Ujerumani, Chancellor ni mkuu wa serikali lakini siyo mkuu wa dola. Kikundi
kilichompendekeza Hilter ateuliwe kuwa Chancellor kilifikiri kuwa kingeweza
kumwendesha kwa urahisi, awe kibaraka wao. Jambo ambalo hawakulitegemea ni
kutumika kwa Jeshi la SA kuzuia
wabunge kuingia bungeni na kupiga kura, mkakati huu ulipelekea kuzuiwa kwa
upinzani bungeni na kurahisisha utawala wa Hitler.
Hitler na Himmler wanakagua Jeshi la SS
Mizizi ya Udikteta
Baada ya muda mfupi Hitler alidai apewe
kifaa cha kisheria cha kumwezesha kutekeleza sera zake, na Sheria ya Kumwezesha (23 na 24 Machi 1933) itapitishwa ambapo
hakuhitajika kuleta kila jambo kujadiliwa mbele ya bunge. Hatua hii ni
ukiukwaji wa taratibu za utawala na zilipelekea kukua kwa udikteta. Inaaminika
kuwa Goring aliwasha moto jengo la bunge, Reichstag tarahe 27 Februari 1933 ili
kuleta msukosuko wa kisiasa na Sheria ya Moto wa Reichstag iliyokabidhi
serikali mamlaka ya bunge. Marinus van
der Lubbe raia wa Holland alisingiziwa kuwa amewasha moto huo kwa hulka
zake za kikomunisti, swala hili lilitumika kuwazuia wabunge wakomunisti kuingia
bungeni na wengi waliwekwa kizuizini.
Kuwa Fuhrer
Mwaka 1934, Hitler aligombania uraisi
dhidi ya Field Marshal Paul von Hindenburg. Hitler alishindwa katika uchaguzi
huu, lakini Hindenburg alipofariki yeye Hitler aliunganisha cheo cha Chancellor
and Rais akawa Kiongozi (Fuhrer). Chama
cha Nazi kilikuwa na wanagambo wake wajulikanao kama Wenye Mashati ya Brown
(Jeshi la Dhoruba), au SA, jeshi hili lilikuwa chin ya uongozi wa Ernst Rohm.
Shida ilijitokeza kuwa yeye Rohm alionekana kama tatizo kwa Hitler na mbinu
zikafanyika akasingiziwa kuwa alitaka kupindia serikali. Rohm na wenzake
waliuwawa kwenye kile kinachojulikana kana Usiku
wa Visu Virefu. Baada ya hapa, Jeshi la SS (Jeshi la Ulinzi) likawa ndiyo
linaongoza katika nyanja zote za usalama na ulinzi wa Hitler. Pia ilimpa nafasi
Heinrich Himmler kupanda cheo na kuwa wanne kutoka kwa Hitler. Wapili alikuwa
Rudolf Hess na watatu Goring.
Horthy na Hitler huko Kiel 1938
Kuanzia mwaka 1935, Hitler alitoa
makucha yake na kupitisha Sheria za
Kibaguzi za Nuremberg. Na mwaka 1936 alipeleka majeshi katika eneo la
Rhineland. Jambo hili lilikuwa limezuiliwa na Mkataba ya Amani wa Versailles wa
1919. Jumuiya ya Madola haikichukua hatua zozote na Hitler akachukulia kama
kibali cha kuanza kujenga jeshi la Ujerumani (Wehrmacht) na kuanza utengenezaji was silaha.
Kumezwa kwa Austria
Ujasiri wa Hitler uliendela kuongezeka,
na mwaka 1938 alilazimisha kuungana kwa Ujerumani na Austria (Anschluss). Baada ya muda, wajerumani wa Sudetenland huko Czechoslovakia
walianza kudai kuwa wananyanyaswa. Malalamiko yao yalikuwa yamepangwa na
viongozi wa ki-Nazi kutoka Ujerumani, kwa kibali cha Mkutano wa Munich ulioitishwa na Mussolini na kuhudhuriwa na Waziri
Mkuu wa Uingereza Neil Chamberlain, Hilter aliteka eneo la Sudetenland la
Czechoslovakia. Kunako tarehe 9 Novemba 1938, Dr Joseph Goebbels alitumia Jeshi
la SA kuharibu maduka ya raia wenye asili ya Kiyahudi na kuchoma masinagogi nchini
Ujerumani kama jibu la mwanafunzi mwenye asili ya kiyahudi kumuua
mwanadiplomasia wa Kijerumani mjini Paris. Uvunjwaji huu wa maduka na biashara
unajulikana kama Usiku wa Vioo vya
Kuchonga. Jambo ambalo halikufikiriwa vizuri na waliopanga udhalimu huu ni
kuwa biashara nyingi zilikuwa zimekatiwa bima, hivyo uchumi wa nchi ulilipia huu
uharibifu wa kupangwa.
Kuanza kwa Vita vya Pili vya Dunia
Huu utaratibu wa kumridhisha Hitler
ulimfanya aendelee kuongeza madai ya ardhi barani Ulaya, na mwaka 1939 alidai
Ujerumani ikabidhiwe eneo la Silesia lililoko Poland na kuwa na kipande cha
ardhi cha kuunganisha Prussia ya Mashariki na Ujerumani kupitia bandari ya
Danzig (Danzig Corridor). Madai haya
hayakukubaliwa na Uingereza na Ufaransa, badala yake nchi hizi mbili zikaweka
Mkataba wa Kudhamini Uhuru wa Poland. Hivyo Ujerumani ilipovamia Poland kunako
saa 11 asubuhi tarehe 1 Septemba 1939, nchi ya Uingereza na Ufaransa viliitaka
Ujerumani iondoe majeshi yake Poland na hadi kufikia tarehe 3 Septemba 1939 na
baada ya Ujerumani kushindwa kutii masharti ya “Ultimatum” ya nchi zote mbili,
dunia ikajikuta katika vita tena.
Hitler na Goring
Kushindwa kwa Ufaransa
Wakati nchi ya Poland inaendelea kumezwa
na Ujerumani na kufuatia Mkataba wa
Molotov Ribbentrop (23 Agosti 1939), Poland Mashariki ilivamiwa na majeshi
ya Kirusi na maafisa 22,000 wa Poland waliuwawa kwa amri za Joseph Stalin,
dikteta wa Kisovieti katika Msitu wa
Katyn. Huku kwenye uwanja wa mapambano wa Ufaransa na Uingereza hakukuwa na
mapigano yoyote na dhana ya “Phoney War”
ikajijenga. Hivi vita vya ukimya viliendelea hadi mwaka 1940 wakati jeshi la
Werhmarcht lilipokuwa tayari kushambulia Ufaransa kupitia Ubeljiji, mbinu ya
kivita ambayo ilitumika pia kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia (Schlieffen Plan).
Jeshi la Wehrmarcht pia lilitumia mbinu ya Shambulio la Radi (Blitzkrieg). Blitzkrieg ilileta
mafanikio dhidi ya Poland na kufikia mwezi June 1940, nchi ya Ufaransa
ilikubali kushindwa na kusalim amri ya Hitler. Hitler aliigawa Ufaransa katika
sehemu mbili, kaskazini ikawa Ufaransa Iliyotekwa (Occupied France) na kusini ikawa Ufaransa ya Kibaraka (Vichy France) chini ya Marchal Petain.
Wakati Ufaransa inasalimu amri ya Hitler, majeshi ya Kiingereza yalitoroka
kupitia bandari ya Dunkirk. Hitler
aliamuru kuwa Mkataba wa Kukubali Kushindwa Vita wa Ufaransa uwekwe sahihi
katika behewa lilelile ambalo lilitumika mwaka 1918 dhidi ya Ujerumani kwenye Msitu wa Compiegne, na baada ya hapo
alilipua lile behewa la treni ili lisije kutumika tena.
Reichsmarschall Herman Goring, Mkuu wa Jeshi la Anga (Luftwaffe)
Pambano la Uingereza
Baada ya Ufaransa kushindwa vita, hatua
iliyofuata ilikuwa kushambulia Uingereza kwa ndege, pambano linalojulikana kama
Pambano la Uingereza (Battle of Britain). Vita hivi vilipiganwa kwa Jeshi la
Anga la Ujerumani (Luftwaffe) kutupa
mabomu kwenye miji ya Kiingereza na Jeshi la Anga la Uingereza (Royal Air Force) kutungua ndege za
kutupa mabomu (Bomber Aircraft) kwa
kutumia mizinga ya ardhini (Anti
Aircraft Machinegun) au ndege za uwindaji (Fighter Aircraft). Ushindi wa Uingereza katika pambano hili
ulitokana na uongozi dhabiti wa Winston Churchill, ndege za Spitfire and ujasiri pamoja na nia ya
wana-anga. Jeshi la Luftwaffe lilikuwa linaongozwa na Reichsmarschall Herman
Goring
Tabaka Tawala
Ilipofika mwaka 1941, Hitler akaamuru
matayarisho ya kuivamia Urusi. Kulikuwa na malengo matatu, la kwanza ni
kuiondoa Urusi kama nchi inayoweza kuwa tishio kwa Ujerumani, pili ni kwamba
Hitler alikuwa anachukia itikadi ya kikomunisti na tatu alitaka ardhi ya Urusi
kwaajili ya kuifanya koloni la Kijerumani (Lebensraum).
Hii ni dhana ya kwamba kuna binadamu wa aina mbili, Herrenfolk (Master Race) inayoundwa na Wajerumani na Wascandinavia.
Wazungu wenye nywele za njano na macho ya bluu. Aina ya pili ni Untermenschen (Sub-human) ambayo ni
nusu binadamu, inayoundwa na watu wengine wote kasoro ya Wafaransa, Waitalia na
mataifa mengine ya wazungu ambao siyo Slavic. Falsafa na itikadi hii
inammanisha kuwa Hitler alikuwa na mpango wa kuwafanya binadamu wote kuwa
watumwa wa Tabaka la Juu. Tarehe 22 Juni 1941 jeshi la Werhmarcht lilivamia
nchi ya Urusi na kufanya maafa makubwa. Siku za mwanzoni za vita Werhmarcht
ilipata ushindi baada ya ushindi na kunako mwaka 1941 walifika karibu na mji
mkuu wa Moscow (Krasnaya Polyana, 28 Novemba 1941, kilomita 29 kutoka Kremlin).
General February
Vita dhidi ya Urusi vilifanya rasilimali
za Ujerumani zitumike kwa kiasi kikubwa sana, hasa kwasababu ya ukubwa wa eneo.
Joseph Stalin aliamuru viwanda vyote vikubwa vilivyopo magharibi vihamishiwe
mashariki, jambo lilichangia uwezo wa Urusi kuendele na vita. Nchi yoyote inayopigana
na Urusi ni lazima izingatie jambo moja muhimu, nalo ni kipindi cha kipupwe
kinachoanza November hadi March kila mwaka. Hivyo jeshi la Wehrmarcht
lililazimika kusimamisha mapigano kwenye kipindi cha kipupwe 1941 / 1942. Jeshi
halikuwa tayari kwa mazingira ya baridi kali, kama ambavyo Napoleone Bonaparte
hakuwa tayari mwaka 1812, miaka 129 iliyotangulia. Ilipofika kipupwe cha 1942 /
1943 ikawa wazi kuwa Ujerumani haitaweza kuiangamiza Urusi, na tarehe 31
Januari 1943 Field Marshal Fredrich von Paulus alisalimisha wanajeshi 93,000 wa
Werhmarcht kwa majeshi ya Urusi. Hitler alimhitaji apigane mpaka askari wa
mwisho atakapo kufa. Na alimpandisha cheo kutoka General kuwa Field Marshal ili
ajiue kuliko kijisalimisha. Kati ya askari 93,000 (au 87,000) waliochukuliwa
mateka Stalingrad Januari 1943 ni 5000 tu ndiyo waliorudi nyumbani baada ya
1945.
Reichsfuhrer SS Heinrich Himmler
Mauaji ya Wayahudi
Kwa maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani,
Reichsfuhrer SS Heinrich Himmler,
kiliitishwa kikao huko Wansee nje ya Berlin kujadili swala la watu wenye asili
ya Kiyahudi. Kama mwanzoni ilifikirika kuwa labda wangeweza kurudishwa
Palestina, na baadaye ikafikirika wangepelekwa Madagascar (Baada ya Ufaransa
kushindwa vita), katika kikao hiki cha 1942 uhamuzi wa kuwaua wote ulikuwa
umeshachukuliwa, na kikao kilikuwa na kazi ya kujadili njia za utekelezaji.
Kuwapiga risasi ilionekana ni kuchezea rasilimali ghali wataki wa vita, na pia
iliwadhuru askari kisaikologia kuua wanawake na watoto. Gesi ya carbon monoxide
haikuwa na ufanisi mkubwa, na pia haikuua watu wote. Hivyo kikao kikashauri
kutumika kwa dawa ya kuua wadudu Zyklon
B yenye cynanide. Kambi za Mauaji
(Death Camps) zikatengenezwa na watu wote ambao walionekana kuwa hawafai
walipelekwa huko kwaajili ya kuuwawa.
Kambi ya Kusindika Watu
Kulikuwa na kambi za aina mbili, ya
kwanza ni Kambi za Kusindika Watu
(Concentration Camps) na aina ya pili ni Kambi za Mauaji. Watu walisafirishwa
na treni kwenye mabehewa ya mizigo (Box Car) bila ya chakula au maji kutoka
kwenye Kambi za Kusindika Watu kwenda kwenye Kambi za Mauaji. Walipofika kwenye
Kambi ya Mauaji, walichaguliwa kwenda kufanya kazi za kitumwa (Forced Labour)
au kwenda kwenye vyumba vya gesi (Gas Chamber). Wazee, watoto, wagonjwa, vilema
na baadhi ya wanawake walipelekwa moja kwa moja kuuwawa. Walivuliwa nguo,
wakakatwa nywele na baadaye kufungiwa kwenye chumba cha gesi ambapo makopo
yenye Zyklon B yalitumbukizwa kwa juu na kutoa gesi ya sumu. Baada ya kelele za
watu kutulia, wafungwa maalum wajulikanao kama Sonderkommando waliitoa ile miili ya marehemu, wakaingoa meno ya
dhahabu au fedha, wakaiweka kwenye matanuru ya moto na kuichoma. Majivu
yalitupwa kwenye mito au yalitengenezea mbole ya chumvi chumvi. Mali za
marehemu zilichambuliwa, na vilivyoweza kutumika vilitumika. Kwa njia hii
takriban Wayahudi million sita waliangamizwa pamoja na Gypsies (Kabila la
Wazururaji wa Ulaya).
Kambi za Mauaji, uchomaji wa miili ya watu.
Nje ya mauaji katika Kambi za Mauaji,
pia kulifanyika mauaji katika misitu huko Estonia, Latvia, Lithuania na
Ukraine. Mauaji haya yalifanya na jeshi la SS, ambapo raia wenye asili ya
kiyahudi na makada ya kikomunisti walivuliwa nguo wakapigwa risasi na kutupwa
kwenye mashimo makubwa (Mass Graves). Na kwa vile jambo hili lilifanyika kwa
uwazi, wale waliokuwa wanasubiri waliona kitakacho wasibu kabla ya kuuwawa.
Vikosi vya Mauaji Einsatzgruppen vilihama kutoka sehemu moja hadi ingine
kutekeleza sera hii ya udhalimu chini ya uongozi wa Reinhard Hydrich. Kinachosikitisha ni kuwa ilipoonekana dalili kuwa
Ujerumani itashindwa vita, Himmler alamuru haya makaburi yachimbuliwe na mateka
wa vita halafu ile miili ichomwe moto kuharibu ushahidi.
Himmler na Jeshi la SS
Kuhodhi Madaraka ya Kijeshi
Mwaka 1943 ulishuhudia Pambano la Kursk,
pambano kubwa la vifaru, mahali ambapo ubora wa kifaru cha Kirusi cha T-34
ulidhihirika. Wakati huu baada ya mabishano mengi na makamanda ya jeshi, Hitler
alitwaa cheo cha mkuu wa jeshi la nchi kavu (Oberster
Befehlshaber des Herres). Alimstaafisha amri jeshi mkuu wa Werhmarcht,
Field Marshal Walter von Brauchitsch (19 Desemba 1941). Awali aliunda Ober Kommando der Werhmarcht (OKW)
chini ya amri yake ikiongozwa na Field Marshal Wilhelm Keitel and Colonel
General Alfred Jodl baada ya kufuta Wizara ya Ulinzi na kumstaafisha waziri wa
ulinzi Field Marshal Werner von Blomberg kunako 4 Februari 1938. Ikumbukwe kuwa
Hitler hakujipansha cheo, alibaki na cheo chake cha Lance Corporal.
Kushindwa Vita
Mwaka 1944, kunako tarehe 6 June,
majeshi wa washirika yalivamia pwani ya Normandy
Ufaransa na kufungua mlango wa mwisho wa utawala wa Hitler, Vita vya Pili
vya Dunia na Dola ya Tatu ya Ujerumani (Third Reich). Vikosi vya vifaru
vilishindwa kudhibiti shambulio hilo hadi Hitler alipoamka saa nane mchana,
jambo lililosaidia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa zoezi hilo la Wamarekani,
Waingereza and Wafaransa. Hitler alitegemea shambulio lingekuja Pas de Calle,
lakini hakuwa hivyo. Licha ya jitihada kubwa, mji wa Paris ulianguka mikononi
mwa Washirika, baada ya hapo uvamizi wa Ujerumani ukaanza. Katika hali hii
Wajerumani walikuwa wanapigana na Warusi kwa upande wa mashariki, Waserbia,
Wakroatia na Wayunani katika peninsula ya Balkan, Waingereza na Wamarekani
katika peninsula ya Italia na Ulaya magharibi. Katika mazingira haya, kikundi
cha mmafisa wa Werhmarcht wakahamua kummua Hitler, Colonel Stauffenberg alitega bomu chini ya meza ya Hitler huko Wolfsschanze Rastenburg Prussia ya
Mashariki tarehe 20 Julai 1944. Kwa bahati kuna mtu alisogeza bomu upande
mwingine was meza na hivyo halikumuua Hitler lilipolipuka. Baada ya hapo
maaskari wengi walinyongwa kulipiza kisasi dhidi ya usaliti huo. Dhoruba hii
ilimkumba pia Field Marshal Erwin Rommel,
kamanda mahiri wa Wehrmarcht huko Afrika ya Kaskazini. Alilazimika kunywa sumu.
Kifo cha Hitler
Kambi ya Mauaji ya Auschwitz ilitekwa na Warusi kunako tarehe 27 Januari 1945, na
baada ya hapo Ujerumani ikaendelea kupoteza ardhi katika kila pambano.
Alipofariki Rais Roosevelt wa Marekani, Waziri wa Propaganda Joseph Goebbels
alisheherekea akifikiri kuwa labda Ushirika dhidi ya Ujerumani ungeyumba,
lakini haikuwa hivyo. Kwasababu ya mabomu yaliyokuwa yanadondoshwa kila siku,
Hitler alilazimika kuhamia kwenye handaki chini ya Reich Chancellery, mahali
ambapo alisheherekea sikukuu ya kuzaliwa tarehe 20 Aprili 1945 na mwishowe
akafunga ndoa na Eva Braun na kujiua
kwa kunywa sumu na kujipiga risasi kunako tarehe 30 Aprili 1945. Siku za mwisho
za Dola ya Tatu zilishuhudia udhalimu dhida ya Wajureumani wenyewe uliofanywa
na Jeshi la SS, ambapo kila mwanaume aliyeshukiwa kuwa ametoroka uwanja wa
mapambano alinyongwa papo hapo, Waziri wa Viwanda Alber Speer aliagizwa alipue
miundombinu yote ili Warusi wasikute chochote cha thamani, Speer hakutekeleza
agizo hili. Herman Goring alituma telegram ya kutaka kuchukua madaraka ya
uongozi, jambo ambalo Goebbels aliligeuza kuwa ni usaliti, Hitler akaamuru
Goring awekwa kuzuizini. Himmler naye alitaka kuwa kujadili kusimamisha
mapigano na Washirika ili ayaendeleze dhidi ya Warusi, kupitia kwa Count Folke Bernadotte, jambo hili
halikufanikiwa, na Hitler alipogundua akaagiza Himmler akamatwe mara moja.
Eva Braun, mke wa Hitler
Uzushi
Joseph Stalin hakutaka kuamini kuwa
Hitler amekufa, hivyo akaendeleza wazo kuwa labda alikimbia. Baada ya Hitler na
Eva Braun kujiua, miili yao ilichomwa moto na lita 180 za petroli na kuzikwa
kwenye bustani ya Reich Chancellery. Warusi walichimbua hiyo miili na baadaye
wakaizika mahali pengine, sehemu ya fuvu la kichwa na taya ya Hitler kilipelekwa
Moscow. Kunako mwaka 1970 miili ilichimbuliwa tena na kutupwa kwenye mto Biederitz
ili kuondoa uwezekano wa kuwa sehemu ya kumsujudu Hitler. Nyumba ya Hitler, Berghof kule Obersalzberg karibu na Berchtesgaden
ilibomolewa na dalili zote kufutwa. Mali zake zote zikakabidhiwa Jimbo la
Bavaria. Vita vya Pili vya Dunia viliisha rasmi tarehe 7 na 8 Mei 1945. Ni
tarehe mbili kwa vile sahihi ya tarehe 7 haikutambuliwa na Warusi itakabidi
zoezi lirudiwe siku inayofuata tarehe 8 Mei 1945.
Matokeo
ya Vita vya Pili vya Dunia
1. Kuundwa kwa Umoja wa Mataifa baada ya
Jumiya ya Madola kushindwa kuzuia vita.
2. Kuwepo kwa ncha mbili katika dunia,
Magharibi ya Ubepari na Demokrasia na Mashariki ya Ujamaa na Udikteta.
3. Kuundwa kwa bomu la Atomiki na kutumika
huko Hiroshima na Nagasaki.
4. Kuzuiwa kwa Ujerumani na Japan
kusababisha vita tena.
5. Kuzinduliwa kwa Tamko la Haki za
Binadamu la Umoja wa Mataifa 1948.
6. Mauaji ya Wayahudi milioni sita.
7. Takriban watu milioni 50 walikufa
kutokana na vita hivi.
8. Kuanzishwa kwa Dola ya Israel 1949.
9. Kusisitizwa kwa itikadi ya watu
kujuhamulia mambo yao wenyewe (Self Determination) na kupelekea uhuru wa
makoloni.
10. Uhuru wa nchi nyingi ulipelekea
maendeleo ya kielimu, kiafya, kijamii na kiteknologia.
11. Vita vilionekana kama udhalimu na
hakujakuwa na vita kubwa tena tangu tarehe 7 / 8 Mei 1945.
12 Kwa kila siku ya siku 1400 ambazo
Urusi ilukuwa katika hali ya vita na Ujerumani, ilipoteza watu 19,000.
23 April 2017
Wahusia Wakuu
1.
Adolf Hitler: Reich Chacellor wa
Ujerumani (Sawasawa na Waziri Mkuu) na baadaye Kiongozi Mkuu wa Ujerumani
(Fuhrer).
2.
Herman Goring: Waziri wa Jeshi la
Anga (Luftwaffe) na Reichsmarschall.
3.
Heinrich Himmler: Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mkuu wa Gestapo (Askari Kanzu) na Reichsfurhrer wa Jeshi la Ulinzi la SS.
4.
Joseph Goebbels: Waziri wa
Propaganda.
5.
Joseph Stalin: Katibu Mkuu wa Cahama
cha Kikomunisti cha Urusi na Kiongozi Mkuu wa Urusi ambaye hakuwa na cheo cha
kiserikali.
6.
Winston Churchill: Waziri Mkuu wa
Uingereza aliyeendesha mapigani dhidi ya Hitler.
7.
Benito Mussolini: Warizi Mkuu wa
Italia.
8.
Vyacheslav Molotov: Waziri wa Mambo
ya Nje wa Urusi.
9.
Joachim von Ribbentrop: Waziri wa
Mambo ya Nje wa Ujerumani.
10.
Eva Braun: Mke wa Hitler.
Vyanzo
1.
Alan Bullock. Adolf Hitler. Iasi. Editura Elit. 2000.
2.
J.P Stern. Hitler: The Fuhrer and the People. Fontana Collins. October 1976.
3.
James Joll. Europe since 1870: An International Histroy. Penguin. 1976.
4.
Nyiszli Miklos. Am Fost Medic la Auschwitz: Morti Fara Morminte, Laboratorul si
Crematoriile Dr-uli Mengele. Editura Aquila 93. 1998.
5.
Dragos Nedelescu. Goebbels Jurnal. Iasi. Editura Elit. 1998.
6.
Marian Podkowinski. Hitler and Archangles of Death. Cluj Napoca. Hiparion.
2001.
7.
Hugh Trevor-Roper. The Last Days of Hitler. 7th Edition. London. Pan
Books. 2012.
Thursday, September 15, 2016
Faida za Boda-boda
Faida za Boda-Boda.
Nilianza kuendesha pikipiki kunako mwaka
1992, ilikuwa Honda C70 iliyotengenezwa mwaka 1980. Kabla ya kutumia pikipiki
safari za mjini zilikuwa ni tatizo haswa kwa vile ni kilometa 3 hadi mjini
katikati na kuna kilima kilichojificha barabara ya Lema, hivyo safari ya kurudi
nyumbani huwa ni ngumu. Wakati jua likiwa kali inabidi kufikiria mara mbili
mbili kabla ya kupanga safari yoyote. Katika barabara hii kulikuwa hakuna
usafiri wa mabasi, isipokuwa yale yaendayo Kibosho Kirima, kama matatu au manne
kwa siku. Niliendelea kutumia hiyo piki piki hadi Septemba 2005 ilipoibiwa.
Kipindi hicho, baada ya kuibiwa nikawa
ninatafuta ingine ya kununua. Kukawa na piki piki za CC 125 kwa sh 600,000 za
kutoka China. Hizi piki piki za bei rahisi zilikuwa dalili ya nafasi ambayo
imekuwa ikijijenga; yaani ajira kwa vijana wa Watanzania. Kuanza kwa biashara
ya usafiri wa piki piki imewapa wananchi fursa ya kuwa na usafiri wa bei nafuu
ambao pia unaweza kupita sehemu ambazo barabara siyo nzuri. Bei ya chombo cha
usafiri ni ndogo, haswa ukilinganisha na bei ya piki piki ya CC 125 ya Honda
ambayo miaka ya 1990 ilikuwa inalingana na Toyota Pick ya tani moja second hand
kutoka Japan.
Kwa sasa, kuna takriban piki piki
1,000,000 hapa Tanzania, ikilinganishwa na takriban magari 880,000. Nchi ya
China imekuwa ikiendeleza vyombo ya usafiri / uchukuzi vidogo kwa muda mrefu. Vyombo hivi ni vya
teknologia rahisi na pia vinaweza kutengenezwa kwa bei ndogo na kuuzwa kwa bei
ndogo. Vyombo ya magurudumu 3 vimekuwa vikitumika huko China kwa muda mrefu.
Swala hili la vyombo vya usafiri vya bei ndogo limepitiwa na nchi za ulaya pia,
haswa baada ya vita vya pili vya dunia. Mifano ni piki piki za Vespa huko
Italia. India waliona faida za piki piki za magurudumu matatu, na ni nchi
inayoongoza kwa usafiri wa vyombo hivyo.
Sisi Watanzania tulianza kugeukia
teknologia rahisi kunako mwaka 1980, wakati trekta dogo (Power Tiller)
lilipotengengenezwa hapa nchini. Baada ya hapo wazo
halikuendelezwa. Hadi kufikia awamu ya nne, ambapo ilikuwa sera ya serikali
kuendeleza matumizi ya Power Tiller kwaajili ya kilimo. Hivyo muongo wa kwanza
(2000 – 2010) umekuwa ndiyo mwamko wa tektnologia rahisi kwa matumizi ya umma
nchini Tanzania, Boda-boda na Power Tiller. Ukijumlisha simu za mkononi na
Solar Power, hizi ndiyo zinazoainisha maedeleo yetu ya sasa.
Maendeleo tutajiletea sisi wenyewe, tukitumia
teknologia zilizopo na haswa zile ambazo zinaendana na mazingira yetu (Appropriate technology), tutaweza
kujijengea maisha mazuri na yenye mfanikio.
Faida za Usafiri wa Piki piki ni hizi:
1. Piki piki ni za bei ya chini.
2. Zinatoa ajira kwa vijana wa Tanzania.
3. Bei ya usafiri ni ya chini.
4. Piki piki zinaweza kufika maeneo
yenye barabara mbovu.
5. Sekta ya Boda-boda inachangia uchumi.
Mapungufu ya Usafiri wa Piki piki ni
hizi:
1. Madereva wa Boda-boda hawana mafunzo
ya udereva.
2. Idadi kubwa ya piki piki hazilipiwi
Motor Vehicle Licence.
3. Idadi kubwa ya piki piki hazilipiwi Third
Party Insurance.
4. Baadhi ya madereva wa Boda-boda
hawana maadili, utu na uadilifu.
5. Vijana wengi wamepoteza viungo na
maisha.
William Makupa
14 September 2016
Subscribe to:
Posts (Atom)